Translate

Friday, June 19, 2020

ENEMY KILLED IN ACTION PART TWO (operation Geronimo)

OPERATION GERONIMO 











CHANJO FEKI

Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Pattena alitaka kwanza kuhakiki kama hisia zao ni za kweli kuwa Bin Laden anaishi kwenye Kasri hilo. Hivyo basi maafisa wa CIA wakaja na mpango kuwa wafanye uhakiki wa uwepo wa familia yake na kama familia yake ipo kwenye jumba hilo basi hapana shaka Bin Laden atakuwepo ndani ya hilo Kasri.

Kwahiyo maafisa hao wakaemweleza mkurugenzi wao wanachotakiwa ni kupata sampuli za vinasaba (DNA) za watoto wanaoishi ndani ya jumba hilo.
Kwahiyo mkakati ukawekwa kwamba ifanyike chanjo feki ili wapate fursa ya kuingia kwenye jumba hilo kuwahudumia watoto na wakifanikiwa kuingia watatumia mbinu kadhaa kuchukua sampuli za vinasaba za watoto eidha kwa kubakiza damu kiduchu za hao watoto kwenye sindano ya kutolea chanjo au mbinu nyinginezo.

Ili kufanikisha azma hii CIA walimuendea Daktari Bingwa aliyeitwa Shakil Alfridi ambaye alikuwa ndiye daktari mkuu katika maeneo ya Khyber mpakani na Afghanistan.

CIA wakafanikiwa kumshawishi daktari Hugo ashiriki kwenye mpango huo wa kutoa chanjo hiyo feki.

Baada ya kufanikiwa kumshawishi Dk. Shakil matangazo yakawekwa kuhusu mpango wa kutoa chanjo katika eneo hilo kwa mwezi February na Mwezi April 2011. Ili kuwapiga chenga serikali ya mji wa Abbattobbad wasihusike kwenye zoezi hilo Dk. Shakil alieleza kuwa amepata ruzuku kutoka mashirika ya kimataifa ili atoe chanjo hiyo bure na chanjo hiyo ni ya kuwakinga watoto dhidi ya Hepatitis B. 

Hivyo basi alifanya zoezi lake kwa Uhuru pasipo kuingiliwa na watu wa serekali za mitaa na manesi ambao walijumuika nae kutoa chanjo hiyo walipata posho iliyoshiba.

Ili kuepuka watu kuanza kuuliza maswali na kuwa na wasiwasi, alianza kutoa chanjo hiyo katika mitaa wanayoishi masikini kama vile mitaa ya Nawa Sher. Alifanya hivyo kwa mwezi February na aliporejea tena alitoa chanjo hiyo katika mtaa wanaoishi watu matajiri katika mji wa Abbattobad yaani mtaa wa Tabil ambapo ndipo kulikuwa na hilo jumba linalotiliwa mashaka.

Ilipofika zamu ya kutoa chanjo kwa watoto waliopo ndani ya hilo jumba walikaribishwa kwa ukarimu na Dk. Shakil mwenyewe akabaki nje getini na akamruhusu nesi aliyeitwa Bakhto aingie ndani ya kasri atoe 'chanjo' kwa watoto.

'Chanjo' ikatolewa, zoezi likaisha Dk. Shakil na manesi wake wakarejea Khyber na kukabidhi sampuli walizozipata kwa CIA.

Sampuli zikasafirishwa mpaka marekani, zikafanyiwa uchambuzi wa DNA kisha ikalinganishwa na DNA ya dada yake Osama Bin Laden aliyefariki dunia mwaka 2010 jijini Boston nchini Marekani kwa uvimbe kichwani.

Baada ya sampuli hizo za DNA kupimwa na kulinganishwa, majibu yakapelekwa mezani kwa Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Pattena. Baada ya Pattena kuyaona majibu hayo akatabasamu mpaka ufizi wa mwisho, akainua simu ya mezani na kupiga ikulu ya Marekani na kuomba kuongea na Rais Obama. 

Mara baada ya kuunganishwa na Rais Obama, Pattena akampa taarifa Rais, taarifa iliyosubiriwa muda mrefu na kwa shauku kubwa, kwa kifupi akamueleza Rais kwa furaha "we got him.!" ("Tumempata.!")

OPARESHENI NEPTUNE SPEAR

Baada ya kupatikana uhakika kuwa Osama Bin Laden anaishi ndani jumba hilo lililopo Abbottabad, CIA wakafanya kikao maalum na Jemedali Msaidizi (Vice Admiral) William H. McRaven ambaye ni kamanda wa kitengo maalum kinachosimamia oparesheni maalum zinazofanywa na majeshi yote ya marekani ( Joint Special Operations Command - JSOC) ambapo katika kikao hicho CIA walimpa taarifa wa kila wanachokifahamu kuhusu makazi hayo waliyoyagundua.

Baada ya kupewa taarifa hiyo, Admiral McRaven akapendekeza kuwa wanaweza wakatuma kikosi cha makomando kufanya uvamizi kwenye jumba hilo lakini akawa na wasiwasi inaweza kuleta mushkeli na jeshi la Pakistan ambalo lipo kilomita moja na nusu tu kutoka makazi ya siri ya Bin Laden.

Baada ya majadiliano ya kina Admiral McRaven akawaagiza maafisa kadhaa kutoka Jeshi la Wanamaji (U.S. NAVY) kitengo cha Maandalizi ya ya Mapigano/vita Maalum ( Special Warfare Development Group - DEVGRU) kwamba waweke ofisi ya muda makao makuu ya CIA Langley na washirikiano kuandaa mpango maalumu utaoenda kupendekezwa kwa Rais juu ya kushugjulikia makazi yaliyoaminika kumficha Osama Bin Laden.

Baada ya miezi miwili ambayo DEVGRU waliitumia kuaandaa mpango kwa kushirikiana na CIA hatimaye wakawasilisha mapendekezo yao kwa Mkurugenzi wa CIA Bw. Pattena na kwa waziri wa ulinzi Bw. Robert Gates.

Kisha Rais Obama akaitisha kikao maalum cha Baraza/kamati ya usalama ya Taifa ili kujadili suala hilo.

Baada ya majadiliano marefu kwenye kikao hicho ilionekana kuwa Rais Obama alipendelea zaidi pendekezo la kulipua makazi hayo kwa bomu kutoka angani. Lakini maswali yakaibuka je ni vipi kama kuna handaki kwenye jumba hilo na Osama labda huwa anakaa chini ya hilo handaki. Katika upelelezi wao wote CIA hawakuweza kung'amua kama kulikuwa na handaki katika jumba hilo ama la.

Kwa kuzingatia hivyo basi (uwepo wa handaki) kama wataamua kulipua makazi hayo kwa bomu basi itawabidi watumie bomu lenye uzito usiopungua Kg. 910 ili liweze kusambaratisha kabisa makazi hayo pamoja na handaki kama lipo.

Lakini pendekezo hili nalo likawa na changamoto zake kwani kama litatumika bomu lenye nguvu kubwa hivyo, kulikuwa na nyumba kadhaa za majirani ambazo zitakuwa ndani ya kipenyo cha mlipuko (blast radius). Pia kama makazi hayo yangelipuliwa kwa bomu kusingekuwa na ushahidi wowote wa kujiridhisha kuwa Osama ameuawa kwenye shambulio hilo.

Baada ya kubainishwa kwa changamoto hizi katika kikao kilichofuata cha kamati ya Usalama wa Taifa, Obama akasitisha mpango huo wa kulipua makazi kwa bomu usitekelezwe.

Chaguo la pili lilikuwa kwa makomando wa kikosi cha Wanamaji (Navy) SEALs, wavamie makazi hayo kwa kutumia helikopta maalum zinazoruka bila kutoa kelele na sio rahisi kuonekana na Rada ya adui. Chaguo hili lilikuwa ni zuri lakini lilikuwa na changamoto moja kubwa. Kumbuka makazi haya yapo karibu kabisa na kituo cha Kijeshi cha Pakistani, itakuwaje kama wakishtukiwa kabla hawajamaliza kutekeleza oparesheni?

Baadhi ya watu waliokuwepo kwenye kikao akiwemo waziri wa ulinzi Bwa. Robert Gates akapendekeza kuwa labda wawashirikishe watu wa kitengo maalumu cha ushushushu cha Pakistan (ISI). Wazo hili likapingwa vikali na Rais Obama kuwa hawaamini hata chembe Wapakistani na endapo wakiwaeleza kuhusu oparesheni hiyo basi siku hiyo hiyo Osama ataamishiwa sehemu nyingine.

Obama akapendekeza kuwa kama ikitokea makomando wao wamekamatwa kabla hawajamaliza oparesheni yao basi Admiral McRaven atatakiwa ajiandae kumpigia simu Mkuu wa Majeshi Pakistani Ashfaq Parvez Kayani kumshawishi kuwaachia makomando hao wa Marekani.

Lakini pia Obama akamuagiza Admiral McRaven awaandae makomando wake kwa mapambano ya kijeshi kama ikitokea wamepewa upinzani na wanajeshi wa Pakistan na hawataki kuwaruhusu waondoke.

Watu wote waliohudhuria kiako hicho cha kamati ya usalama wakakubaliana na mpango huo wa kuvamia makazi ya Bin Laden kwa kutumia helikopta isipokuwa Makamu wa Rais Joe Biden pekee aliupinga mpanga huo kwa asilimia zote.

Licha ya Makamu wa Rais kuupinga mpango huo, siku ya tarehe 19 April kamati ya Usalama wa Taifa ilipokutana tena Rais Obama akatoa idhini ya awali kukubali oparesheni hiyo itekelezwe. Na ikapewa jina Oparesheni Neptune Spear.

Kesho yake McRaven pamoja na kikosi chake cha SEALs wakaondoka marekani kuelekea Afghanistan ambapo walitumia takribani wiki mbili kufanya mazoezi kuhusu oparesheni waliyoenda kuifanya.

Kikosi hiki kilifikia katika kambi ya Bagram nchini Afghanistan na hapo palitengenezwa mfano wa nyumba kama ile inayosadikiwa kumuhifadhi bin laden na kikosi cha SEALs wakafanya wazoezi ya kutosha jinsi watakavyotekeleza zoezi hilo.

Ilipowadia siku ya tarehe 29, Rais Obama alimpigia simu Kamanda McRaven kumuuliza juu ya maendeleo ya maandalizi. Pia akamuuliza kama alikuwa na angalau ya chembe ya shaka kuhusu kufanikiwa kwa oparesheni hiyo na kama alikuwa na shaka yoyote basi oparesheni hiyo itahairishwa. McRaven akamjibu kuwa vijana wake wako tayari kwa kutekeleza Oparesheni.

Obama akawapa idhini ya mwisho kuwa amewaruhusu kufanya oparesheni hiyo siku itakayofuata yaani tarehe 30 April.

Kesho yake Obama akataarifiwa kuwa oparesheni imehairishwa kwa muda wa siku moja kutokana na hali ya hewa kutokuwa rafiki na badala yake itafanyika kesho yake tarehe 1.

Jioni ya siku hiyo Obama akampigia simu tena McRaven kumtakia kilala kheri yeye na makomando wake wa SEALs na akwashukuru kwa kujitoa kwao kwa ajili ya Taifa lao.

Siku ya tarehe 1 May ilipowadia wajumbe wa kamati ya usalama wa taifa walikusanyika katika chumba maalumu cha ikulu ya marekani (situation room) kufuatilia oparesheni hiyo kupitia kwenye runinga iliyokuwa inaonyesha picha za moja kwa moja zilizokuwa zinachukuliwa ndege ya kujiendesha (drone) iliyokuwa inafuatilia tukio zima la oparesheni hiyo.

Usiku wa manane Makomando wa SEALs wapatao 79 waliruka na helikopta za kijeshi kutokea kambi ya kijeshi ya Bagram mpaka eneo la mpakani Jalalabad. Walipofika hapo wakagawana. Makomando wapatao 24 pamoja na mbwa aina ya Belgia Malinois aliyeitwa Cairo waliingia kwenye helikopta mbili aina ya Black Hawk ambazo zimeboreshwa kuzuia kuonekana na Rada ya adui na kutotoa sauti.

Makomando waliosalia waliingia kwenye chopa kubwa za kijeshi aina ya Chinook.

Makomando ambao walipanda kwenye chopa za kivita aina ya Black Hawk hawa ndio walipewa jukumu la kuvamia makazi ya Bin Laden. Makomando wengine ambao walipanda kwenye chopa kubwa za kivita aina ya Chinook hawa watakaa maili kadhaa kutoka eneo la tukio kama tahadhali ikitokea wenzao wakahitaji msaada zaidi.

Baada ya kujigawanya hivi safari ya kuelekea kwenye makazi ya siri ya Bin Laden ikaanza.

Baada ya kuyafikia makazi ya Bin Laden Chopa moja ilitua eneo la mbele ya jengo na nyingine ilitua nyuma kwa juu na makomando wakashuka kwa spidi ya haraka kwa kutumia kamba.

Chopa ambayo ilitua mbele ya jengo, rubani aliiweka chini kwa makosa kidogo na kusababisha mkia wa helikopta kugonga uzio wa ukuta wa nyumba na almanusuura ipinduke chini juu lakini kwa ustadi akaiweka sawa na makomando wakashuka salama ingawa helikopta tayari ilikuwa imeharibika.

Baada ya makomando wote kufanikiwa kuingia ndani ya uzio wakaanza kuisogelea mlango mkubwa wa nyumba. Pembeni ya nyumba kubwa kulikuwa na vyumba vichache vimejengwa kwa ajili ya wageni na ndani yake walitokea wanaume wawili waliokuwa na bunduki aina ya AK-47 na kuwafyatulia risasi makomando wa SEALs. 

Kabla watu hao hawajaleta madhara yoyote makonmando wa SEALs waliwadondosha chini kwa risasi mbili kila mmoja. Watu hawa wawili walikuja kutambulika baadae kuwa ni Abu Ahmed al-Kuwait pamoja na kaka yake aliyeitwa Abrar.

Kisha makomando wakaingia ndani ya nyumba. Na baada ya kuingia ndani kuna kijana akaonekana akikimbia kupandisha ngazi kwenda ghorofa ya juu. Naye akadondoshwa chini kwa risasi. Kijana huyu naye alikuja kutambulika kama mtoto mkubwa wa kiume wa Osama Bin Laden. 

Baada ya kijana huyo kupigwa risasi mlango wa chumba kilichopo ghorofa ya juu ulionekana kufunguliwa na mtu akachungulia. Pia naye akafyatuliwa risasi kadhaa zikamkosa lakini moja ikampata ubavuni. Mtu huyo aligeuka haraka na kurudi ndani chumbani lakini kabla hajaufunga mlango wa chumba vizuri komando wa SEALs alifanikiwa kuruka na kubiringika mpaka ndani ya chumba hicho. 

Katika kujitahidi kujificha mtu huyo (Bin Laden) alimnyakua mwanamke mmoja aliyekuwepo humo chumbani (mkewe Mdogo) na kumsukumia kwa komando wa SEALs lakini komando alifanikiwa kumkwepa mwanamke huyo na akafanikiwa kufyatua risasi iliyompata Osama kwenye paji la uso. 

Papo hapo komando mwingine naye alikuwa ameshaingia chumbani naye akafyatua risasi iliyompata Osama kifuani. Bin laden akadondoka chini na komando mmoja akamfyatulia risasi nyingine kifuani akiwa hapo hapo chini. Pale pale roho ya Osama Bin Laden ikaach mwili.

Komando mmoja akatoa simu ya mawimbi ya kijeshi na kuwasiliana na kamanda McRaven aliyekuwa amebaki kwenye kambi ya Bagram. Baada ya kupokea tu simu komando akamueleza kamanda wake kwa kifupi tu "Geronimo". 

Kamanda wake nae akaitafsiri taarifa hii kwa watu waliopo Ikulu marekani pamoja na Rais Obama wakifuatilia Kupitia Satelaiti, kamanda McRaven akawaeleza "For God and for the country, Geronimo Geronimo Geronimo" kisha akamalizia "Geronimo EKIA" (EKIA - Enemy Killed In Action (Aduai ameuawa kwenye mapambano)). Geronimo ndio lilikuwa jina la fumbo (code name) la kumtambua Osama Bin Laden katika oparesheni hii.

Seneta Hillary Clinton kipindi akiwa kama waziri wa mambo ya nje wa Marekani naye siku alikuwepo Ikulu ndani ya situation room anaeleza kuwa mara baada ya Rais Obama kusikia taarifa hii kwa msisimko na hisia kubwa akaongea maneno machache tu, "we got him" ("tumempata/tumemmaliza").

Baada ya kutoa taarifa hiyo kuwa wamefanikiwa kumuua Bin Laden, makomndo wa SEALs wakawakusanya wanawake na watoto wote waliowakuta ndani ya nyumba hiyo na eakawafunga kwa pingu za plastiki na kuwaacha hapo hapo. Kisha wakaubeba mwili wa Bin Laden na kuupakia kwenye Chopa. 

Lakini kabla ya kuondoka wakailipua ile chopa iliyopata itilafu kwani isingeweza kuruka tena na hawakutaka watu wajue teknolojia yao ya siri inayotumika kwenye chopa hizo. 

Zoezi lote hili lilipangwa kutumia dakika 40, lakini kutoka na umahiri wa hali ya juu wa makomando wa SEALs liliisha ndani ya dakika 30 pekee. Risasi 16 tu ndizo zilifyatuliwa na watu 5 waliuwawa (Osama, mtoto wake wa kiume, Abu Ahmed al-Kuwait, Abrar (kaka wa al-kuwait), na mke wa Abrar).

Baadaya ya hapo wakaruka mpaka kambi ya Bagram kisha mwili wa Bin laden ukapakiwa tena kwenye chopa na kupelekwa kwenye manowari ya kivita ya NAVY iliyoko baharini. Huko sampuli za DNA zikachukuliwa na mwili ukapigwa picha. Baada ya hapo mwili ukavilingishwa shuka jeupe alafu ukatumbukizwa kwenye mfuko mkubwa na imara, vikawekwa na vyuma vizito ndani yake, mfuko ukafungwa, ukatumbukizwa baharini. Huo ukawa mwisho wa Bin laden Duniani.

HOTUBA YA UTHIBITISHO

Jioni ya siku hiyo Rais wa marekani Barack Obama alitoa hotuba ambayo itakumbukwa kwa vizazi vingi vijavyo. Alisema;

"Habari za jioni, usiku huu napenda kuwataarifu Wamarekani na Ulimwengu wote kuwa Marekani imeendesha oparesheni iliyofanikiwa kumuua Osama Bin Laden kiongozi wa Al Qaeda na Gaidi anayehusika na vifo vya maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia......"

Ulimwengu ulisimama kwa sekunde kadhaa na wengine hawakuamini masikio yao na mpaka sasa wapo wasio amini na kumeibuka nadharia nyingi mno. Lakini hiki nilichokisimulia ndicho wanachoamini CIA na serikali ya Marekani, kuwa siku ya Tarehe 1 mwezi May mwaka 2011; "Geronimo EKIA"..... Adui aliuwawa katika mapambano.

Na huo ndio ukawa mwisho wa Osama Bin Laden. Lakini nani wa kuamini hilo? Kuwa Osama Bin Laden aliuwawa kwenye operation hii? Nje ya yote Dunia ilikuja kuamini kuwa Osama Bin Laden aliuawa kweli kwenye operation hii pale ambapo mwanaye Hamza Bin Laden na kundi la Al-Qaeda walipo kuja kuthibitisha hilo hapo baadae.

No comments:

Post a Comment

SIXBERTY MANSON POSTS

Mona Lisa

  MONALISA                              LA GIOCONDA                          By Sixberty Manson  A picture by Sixberty Manson  MEET THE REAL...

ZILIZOTAZAMWA ZAIDI